music

HANS%20MBEDULE%20BLOG

Thursday, February 7, 2013

Arusha; Njaa yasababisha wanaume kutelekeza familia

 

WAKATI njaa ikizidi kuathiri maeneo mbalimbali nchini, baadhi ya wanaume katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha wamekimbia familia zao kutafuta chakula.
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa baadhi ya wanaume wameshindwa kuhudumia familia zao na kulazimika kwenda nchini Kenya na baadhi ya mikoa nchini kusaka vibarua.
Mwandishi wa gazeti hili alifanya mahojiano na baadhi ya wakazi wa eneo hili wakiwamo wanawake ambao wanaelezea hali ilivyo.
Jirani na Bibi Lembirika nakutana na msichana mwenye umri kati ya miaka 15 hadi 19 anajitambulisha kuwa ni  Narik Saruni, mgogoni ana mtoto mdogo, Grace Noah.
Nalazimika kumuuliza baba yake na mtoto yupo wapi, anajibu kwa Kiswahili cha taabu kuwa amekwenda kutafuta kazi ya ulinzi nchini Kenya.
Narik mkononi, ana mfuko na ninapomuuza ana nini, anajibu kuwa ana mboga za porini anauza kila fungu moja Sh100. Anajieleza kuwa akipata pesa hizo, ananunua mahindi na kusaga ili kupata uji wa kunywa yeye  na mtoto wake.
“Kila siku nakwenda porini kuchuma mboga na nikipata naleta huku  madukani kuuza kwa siku naweza kupata Sh800 ambayo naitumia kununua kopo moja la mahindi,”anasema.
Familia zaishi kutegemea mchicha pori
Nakwenda katika Kijiji cha Irkepus,Kata ya Nainokanoka, hapa nakutana na kundi la watoto, wakiwa na bibi zao na mboga za majani mkononi, nasimama na kuwaliza, lakini hawajui Lugha ya Kiswahili.
Hapa nampata Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Irkepus, Thomas Ole Njoro anamwita mmoja wa wanawake hao ambaye anajitambulisha kwa Kimasai kuwa ni Topoi Lembaya ila hajui miaka aliyozaliwa. Hata hivyo, kwa kumtazama ni bibi kizee mwenye umri kati ya miaka 75 hadi 85, kwani hata kutembea kwake anatumia fimbo. Kupitia mwenyekiti huyo wa kitongoji nawauliza, walichobeba ni nini, bibi huyo anajibu kwa Kimasai kuwa ni mchicha wa porini ambao wanachuma kwa ajili ya chakula.
Anasema hayo ndio maisha yao kwa takriban mwezi sasa kwani, mahindi ya msaada ambayo yalitolewa na Serikali hivi karibuni pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wamemaliza, hivyo hawana chakula tena.
Bibi huyo anasema anaishi na wajukuu hao, kwani baba yao, Lesika Lemoro ameenda nchini Kenya kutafuta kazi.
Familia nyingi ambazo ninazitembelea ninakutana na wanawake na watoto huku wanaume wakielezwa kuwa wameondoka kwenda Kenya na Arusha na mikoa mingine kutafuta kazi. Mpaka wa Kenya upo jirani na vijiji hivi.
Anasema maisha yao ni taabu, kwani hawana ng’ombe na sasa wamegeuka ombaomba katika maboma ya jirani. Mwenyekiti huyo wa Kitongoji, anakiri familia hiyo, kukabiliwa na njaa kwani anasema Desemba 20, mwaka jana ndiyo ilikuwa mara yao ya mwisho kupata chakula cha njaa.
Anasema katika kitongoji chake, kaya 379 zinakabiliwa na upungufu wa chakula, lakini ni kaya 125 tu ndizo zilipatiwa chakula kiasi cha kilo tisa za mahindi kwa kila kaya.
Mahindi ya kuchemsha yaokoa familia
Natembea kwenye maboma ya Kimasai katika kijiji hicho, naingia kwenye moja ya maboma haya napiga hodi hakuna ambaye anaitika, lakini naingia ndani nakutana na moshi mkali.
Hapa nabaini kuwa kuna watu, lakini kutokana na nyumba za jamii hii za kimasai kuwa za asili, zenye vidirisha vidogo sana, nashindwa kuvumilia na kutoka nje na ndipo bibi kizee anatoka ndani.
Nashindwa kuzungumza naye na hapa pia nalazimika kumwita Mwenyekiti wa kitongoji ili aje kuwa mkalimani, anafika na kumuuliza bibi anafanya nini ndani. Bibi huyu mwenye umri kati ya miaka 80 hadi 90 akiwa haoni, anajitambulisha kuwa ni Saleita Nanga, anasema anapika chakula cha wajukuu wake wanne.
Hapa napata shauku ya kuomba nikione chakula hicho, Mwenyekiti wa kitongoji analazimika kuingia ndani ya boma hili na anatoka na sufuria yenye mahindi yanayocheshwa.
Hapa nabaini ni mahindi ambayo hayajachanganywa na kitu yametoka kwenye magunia na moja kwa moja kuingizwa katika maji machache na kuchemshwa.
Nanga anasema hicho ndio chakula cha siku hiyo na muda huo ni saa 11:30 jioni anasema wajukuu zake, tangu wanywe chai asubuhi hawajaonja kitu kwani hana uwezo wa kupata chakula zaidi ya mara mbili.
Chakula cha msaada chashindwa kusambazwa
Katika kijiji hiki pia nakutana na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kipenjiro,Saiboko Kimirei ambaye eneo lake ndio linatajwa kukabiliwa  kuna wananchi wengi wanaokabiliwa na njaa kali.
Kimerei anasema hali ya usambazaji wa chakula katika eneo lake ni gumu kwani maeneo mengi barabara hazipitiki kabisa.
“Kwangu hali ni mbaya sana, ukifika unalazika kutembea kwa miguu hadi kilomita 20 kuonana na wananchi kwani hakuna barabara ya gari,” anasema Kimerei.
Anasema tayari ametoa taarifa ngazi za serikali juu ya hali hiyo na ugumu wa kusambaza chakula, lakini bado hajapewa majibu ya uhakika.
Ofisi ya Waziri Mkuu yawaokoa Enduleni
Siku ya pili mapema asubuhi, nakwenda katika Kata ya Enduleni kata hii ndio anatoka Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Saning’o Ole Telele.
Hapa napokelewa na sura za matumaini za wanawake, vijana, watoto na wazee, kwani siku hiyo, walikuwa wanapokea chakula cha msaada kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, kiasi cha tani 70 za mahindi.
Mwenyekiti wa kijiji hiki, Julius Peter anasema, wamepokea tani 70 za mahindi ambayo wanauza Sh50 kwa kilo moja.  Hapa ni heka heka ya kugawana mahindi tu na wakati zoezi likiendelea naona makundi ya watoto wenye makopo wakizoa chini, mahindi kidogo yanayomwagika.
Hawa ni watoto wa jamii ya kimasai na wanazoa mahindi huku, wakigombania na hivyo nabaini pia katika eneo hili hali ya uhaba wa chakula ipo.
Nalazimika kuhojiana na makundi mbalimbali ya wanawake na vijana na hapa, nampata Mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake wa CCM wa Kata hiyo ya Enduleni, Emilisiana Munga.
Munga anasema, kata hiyo yenye watu zaidi ya 12,000  nusu yao wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

No comments:

Post a Comment